Miembe yenye Miaka 100 inavyowatesa wakazi Morogoro, Historia yake yaanikwa
Автор: Mwananchi Digital
Загружено: 2024-11-05
Просмотров: 2215
Описание:
Wakazi wa mtaa wa Boma Road, manispaa ya Morogoro, wameeleza historia ya miti ya miembe yenye zaidi ya miaka 100 iliyopandwa enzi za utawala wa Wajerumani.
Wakisimulia hadithi walizorithishwa na mababu zao, wakazi hao wamesema miembe hiyo ilipandwa kama sehemu ya uhifadhi wa mazingira na pia kama adhabu kwa watu walioonekana kukosea wakati huo.
Wajerumani walitawala Tanganyika kuanzia mwaka 1889 na kujenga maboma katika baadhi ya mikoa, ikiwemo Morogoro. Ili kupendezesha maeneo ya maboma yao, walipendelea kupanda miti kwenye barabara zinazoelekea maboma hayo.
Barabara maarufu ya Boma Road, inayoingia mpaka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ni mojawapo ya maeneo yenye historia ya miembe hiyo.
Kwa mujibu wa Sudi Ramadhan Kiroboto, mkazi wa Boma Road, miembe hiyo imekuwa sehemu ya maisha yao kwa muda mrefu, ikiwa na faida kama kivuli, matunda, na mandhari nzuri. Kiroboto alisema,
"Tumeikuta hii miembe, na kweli imetulea, kwasababu tumekula sana matunda yake na tunapata kivuli kizuri tunapopumzika nje."
Wakazi wanaeleza kuwa, zamani, miembe hiyo ilikuwa na mavuno mengi, na matunda yake yaliwasaidia baadhi ya watu kupata kipato, Hata hivyo, kutokana na umri mkubwa wa miti hiyo, uzalishaji wa matunda umepungua, Pia, matawi ya miembe hiyo yamekuwa yakianguka mara kwa mara, hasa wakati wa mvua na upepo mkali, hali inayosababisha hasara kwa nyumba na miundombinu ya umeme.
Kiroboto anaeleza kuwa wakazi wa Boma Road wamewahi kutoa malalamiko kwa serikali kuhusu hatari inayoweza kusababishwa na miembe hiyo, na walishauriwa kupunguza matawi, lakini gharama yake ni kubwa.
Issa Mkwembo, mkazi mwingine, alisema kuwa miembe hiyo inabeba historia na inawakumbusha madhara ya ukoloni, akiiomba serikali kuipunguzia matawi mara kwa mara ili isilete madhara kwa jamii.
"Miembe hii ni historia na ni alama ya madhara ya ukoloni wa kijerumani, na vizazi vijavyo vinapaswa kujifunza kupitia mifano hii hai, hivyo, ni vyema serikali iangalie namna bora ya kuitunza na kuipunguzia matawi kila baada ya muda," alisema Mkwembo.
Mwananchi ilifika ofisi ya Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira katika manispaa ya Morogoro kujua mikakati ya serikali katika kuhakikisha miembe hiyo haitaleta madhara kwa jamii.
Dawson Jeremiah, mkuu wa kitengo hicho, alisema kuwa serikali haina mpango wa kukata miembe hiyo kwa kuwa ina thamani ya kihistoria na pia inapendezesha barabara hiyo maarufu ya Boma Road.
"Kwanza kabisa, hatuna mpango wa kukata hii miembe, licha ya kuwa ni historia lakini pia inapendezesha barabara yetu inayoanzia stendi ya zamani ya Hice mpaka ofisi za Mkuu wa Mkoa," alisema Jeremiah.
Aliongeza kuwa miti hiyo ina uwezo wa kuishi kwa muda mrefu kutokana na aina ya mbegu zilizopandwa enzi za Wajerumani, ambazo zinahimili mazingira na kuishi kwa muda mrefu.
Alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuacha kulundika takataka kwenye mashina ya miembe na kuzichoma moto kwani tabia hiyo inadhoofisha miti na kuifanya ianguke.
"Kwa kushirikiana na ofisi ya kata, tuna taratibu za kushughulikia matawi yanayoonyesha dalili za kuanguka kwa kutoa taarifa na kuyashughulikia mara moja," alieleza Jeremiah.
Повторяем попытку...
Доступные форматы для скачивания:
Скачать видео
-
Информация по загрузке: