TAFAKARI YA SIKU ALHAMISI YA JUMA LA 3 MWAKA C 31/01/2019
Автор: KANISA KATOLIKI TANZANIA TEC
Загружено: 2019-01-30
Просмотров: 1619
Описание:
#Mt.YohaneBosko
WAPENDWA TAIFA LA MUNGU TUMSIFU YESU KRISTO!
KARIBUNI KATIKA TAFAKARI YA SIKU: TAREHE 31/01/2019
(Alhamisi ya Juma la 3 la Mwaka) KUMBUKUMBU YA MT. YOHANE BOSKO
WAZO KUU: KUTENDA MEMA
SOMO LA INJILI ILIVYOANDIKWA NA MT. MARKO 4:21 – 25
Akawaambia, “Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.” Akawaambia, “Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakacho pimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alichonacho atanyang’anywa.”
NENO LA BWANA…
Wapendwa Taifa la Mungu!, katika Injili tuliyoisikia hivi punde, Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha sisi tulio wafuasi wake, kwa sacramenti ya Ubatizo tumepewa wajibu wakutekeleza, yaani kuweka taa juu ya kiango ili kuumulika ulimwengu wenye giza. Anatumia neno taa yaani Mwanga akimaanisha Neno la Mungu, kama Mzaburi anvyotufundisha “Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu” (Zab 119:105).
Pia Neno Mwanga lina mwakilisha Kristo mwenyewe kama anavyo jitambulisha “Mimi ndimi nuru ya ulimmengu yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe” (Yn 8:12) hayo ni maneno yake Kristo tunayo ambiwa, kusudi tupate kufuata mwenendo wake na desturi zake tukitaka kweli kuweka taa juu ya kiango. Basi bidii yetu kubwa sharti iwe kujifunza maisha ya Yesu kristo aliye Nuru ya Ulimwengu.
Kwa kawaida taa ikiwekwa mvunguni giza hutawala, vivyo hivyo Neno la Mungu lisipo dhihirika, giza hutawala, giza linalo maanishwa hapa ni dhambi na mizizi yake.
Wapendwa Taifa la Mungu, Ulimwengu wa leo unahitaji kuangazwa ili kuondoa giza la dhambi hasa katika ngazi ya Familia ambayo ni shule ya malezi msingi kwa mwanadamu: kunaweza kuwapo magomvi, kutoaminiana, kuhisiana vibaya, na kusemana ovyo mitaani. kuzembea katika kutimiza wajibu zetu hasa wazazi katika jukumu la malezi kwa kisingizio cha kazi nyingi. Tabia za waume kuwatesa wake zao na baadhi ya wake kuwatesa waume zao. Je! sio kuweka taa mvunguni huko?
Katika jamii tunamoishi kuna giza la dhambi giza hilo ni matendo ya: uuwaji wa vikongwe, uuaji wa mimba, wizi wa aina mbalimbali kwa mfano: Vitendo vya rushwa, kuhujumu uchumi na ufisadi. Pia kuna dhambi ya uharibifu wa mazingira yaani “Nyumba ya wote” kama tunavyo fundishwa katika waraka wa kitume ‘Laudato Si’ wa Baba Mt. Francisko. Je! Mambo kama hayo sio kuweka taa mvunguni?
Wapendwa Taifa la Mungu, tunaalikwa kuachana na vitendo vya giza kwa maana “…zamani ninyi mlikua giza, bali sasa mmekua nuru katika Bwana enendeni sasa kama watoto wa nuru” (Eph 5:8).
Hivyo sisi tuliowafuasi wa Kristo kwa njia ya ubatizo, tunaagizwa kutangaza neno la Mungu, tuchangie kuleta mwanga wa hali Njema katika Familia ya mwanadamu na jamii inayotuzunguka ili kuweka taa juu ya kiango yaani kulidhihirisha neno la Mungu kwa kulitangaza na kuliishi.
➢ Angalieni msikialo: yaani tutilie maanani yale tunayosikiliza, yatusaidie kuzaa matunda mema.
➢ Angalieni kipimo kile mpimacho ndicho mtakacho pimiwa: kwamba kadiri tunavyo fanya jitihada kulisikiliza Neno la Mungu na kuliishi kadiri hiyohiyo tunapata msaada wa neema ya Mungu.
➢ Wapendwa Taifa la Mungu, tumuombe Mungu atujalie bidii ya kusikiliza na kutenda mapenzi yake, hivyo tuweke Taa juu ya kiango ili watu wayaone matendo yetu mema na wamtukuze Mungu.
TAFAKARI HII IMETOLEWA KWENU NA FRT. DAUDI MAKUNGU WA JIMBO KATOLIKI SUMBAWANGA, MWAKA WA TATU WA TEOLOJIA KATIKA SEMINARI KUU KIPALAPALA - TABORA
Повторяем попытку...
Доступные форматы для скачивания:
Скачать видео
-
Информация по загрузке: